No title


 RAIS wa Kenya, William Ruto amewataka Wakenya wabadili mtazamo wao kuhusu Watanzania. Amesema mataifa hayo mawili si maadui bali ni ndugu wanaounganishwa na historia, biashara na ushirikiano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC). Rais Ruto alisema hayo akiwa na mwenyeji wake Rais Samia Suluhu Hassan kwenye Jukwaa la Biashara kati ya Tanzania na Kenya, Dar es Salaam juzi. 

“Sisi si maadui. Kenya na Tanzania si maadui. Maadui wetu wa kweli ni umasikini, ukosefu wa maendeleo na ukosefu wa ajira,” alisema Rais Ruto. Alisema ni muhimu kwa wananchi wa nchi zote mbili kuelekeza nguvu katika kujenga uchumi badala ya kushindana kwa misingi isiyo na tija, akisisitiza kuwa ushirikiano wa kikanda ndio njia sahihi ya kufanikisha maendeleo ya pamoja.

 Alisema kuna haja ya kubadilisha fikra zinazoweza kuathiri mahusiano ya kibiashara akisema baadhi ya mifano ya malalamiko kuhusu uwekezaji kati ya pande hizo mbili inapaswa kuangaliwa kwa mtazamo wa fursa badala ya vikwazo. Rais Ruto alisisitiza biashara kati ya Kenya na Tanzania imeendelea kukua, na kutaja uwekezaji wa Kenya nchini Tanzania umefikia zaidi ya Dola za Marekani bilioni 1.7 na wa Tanzania nchini Kenya ukifikia zaidi ya Dola za Marekani milioni 330 katika sekta mbalimbali. 

Pia, alisema licha ya mafanikio hayo, bado kuna changamoto za vikwazo visivyo vya kikodi na urasimu mipakani vinavyopaswa kuondolewa ili kurahisisha biashara na kuongeza mapato ya pande zote mbili. Rais Ruto aliyekuwa nchini kwa ziara ya kitaifa ya siku mbili alisisitiza umuhimu wa kuimarisha miundombinu ya kikanda ikiwamo reli, bandari na miradi ya nishati.

BOSS TV

Hii ni Official blog ya BOSS MEDIA kwa habari za siasa, jamii, elimu, burudani na michezo tufuatilie kwa uhakika zaidi

Post a Comment

Previous Post Next Post