BILA AMANI HAKUNA MAENDELEO KABISA

BILA AMANI HAKUNA MAENDELEO KABISA

Size
Price:

Read more

 

 


Katibu wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Kenani Kihongosi, amewataka wananchi wa Wilaya ya Karatu mkoani Arusha kuendelea kulinda amani na utulivu uliopo ili kuhakikisha shughuli za kiuchumi na maendeleo zinaendelea kustawi katika eneo hilo.

Akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika Karatu, Kihongosi amesema amani ndiyo nguzo kuu inayowezesha wananchi kufanya biashara, kulima, kuendesha shughuli za utalii pamoja na kazi za usafirishaji ikiwemo bodaboda na bajaji.

Amesema uwepo wa maelfu ya wananchi waliojitokeza kwenye mkutano huo ni ushahidi kuwa wilaya hiyo inaendelea kuwa na mazingira ya amani na utulivu, akibainisha kuwa hali hiyo ikitoweka sekta mbalimbali za uchumi zitaathirika kwa kiwango kikubwa.

Kihongosi amesisitiza kuwa jukumu la kulinda amani si la vyombo vya dola pekee, bali ni wajibu wa kila mwananchi kuhakikisha anashiriki katika kudumisha mshikamano, umoja na maelewano ndani ya jamii.

Ameeleza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, imeendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo nchini, jambo ambalo limewezekana kutokana na kuwepo kwa mazingira salama na yenye utulivu.

Kwa mujibu wa Kihongosi, wilaya ya Karatu ni moja ya maeneo muhimu kiuchumi kutokana na shughuli za utalii, kilimo na biashara, hivyo ni muhimu wananchi wakaendelea kushirikiana katika kulinda rasilimali na mazingira yanayochochea ukuaji wa uchumi.

Aidha, amewahimiza vijana kutumia fursa zilizopo kujiajiri na kushiriki kikamilifu katika shughuli za uzalishaji mali badala ya kujiingiza katika vitendo vinavyoweza kuhatarisha usalama na maendeleo ya jamii.

Katika mkutano huo, wananchi walipata fursa ya kueleza changamoto mbalimbali zinazowakabili pamoja na kutoa maoni kuhusu masuala ya maendeleo, huku Kihongosi akiahidi kuwa chama na serikali vitaendelea kuzifanyia kazi hoja hizo kwa lengo la kuboresha maisha ya wananchi na kuimarisha maendeleo ya Wilaya ya Karatu.

0 Reviews

Contact form

Name

Email *

Message *