Read more
MKUU wa Wilaya ya Shinyanga, Julius Mtatiro, amesema utulivu na amani
iliyopo nchini Tanzania imeendelea kuwa kivutio kikubwa kwa wawekezaji
kutoka mataifa mbalimbali kuja kuwekeza katika miradi ya maendeleo yenye
manufaa kwa wananchi.
Mtatiro
ametoa kauli hiyo baada ya kutembelea mradi wa maji uliotekelezwa
katika Kijiji cha Zumve, Kata ya Nyamalogo, Wilaya ya Shinyanga. Ametoa
wito kwa wananchi kuendelea kushirikiana na serikali katika kulinda
amani na kudumisha mazingira yanayowezesha maendeleo kupatikana.
Amesema
wananchi wanapaswa kuwa raia wema kwa kutekeleza wajibu wao, kufanya
kazi kwa bidii, kushirikiana na serikali pamoja na kuhoji kwa njia
sahihi ili kuhakikisha serikali inatimiza wajibu wake kwa wananchi.
“Tunapoendelea
kuwa wananchi wema, tukifanya kazi kwa bidii, kushirikiana na serikali
yetu na kuihoji kwa njia sahihi ili itimize wajibu wake kwa wananchi,
huku tukilinda amani yetu, tutaendelea kuvutia wawekezaji wengi zaidi,”
amesema Mtatiro.
Aidha,
amesisitiza kuwa wawekezaji hawawezi kupeleka mitaji yao katika nchi
zenye migogoro na ukosefu wa utulivu, hivyo amani ni rasilimali muhimu
inayopaswa kulindwa na kila Mtanzania wakati wote.
“Hawawezi
kupeleka uwekezaji kwenye nchi zenye migogoro. Amani ni jambo la msingi
sana kwa maendeleo ya taifa letu, hivyo tuilinde mchana na usiku,”
amesisitiza.
Mtatiro
ameongeza kuwa ulinzi wa amani utaendelea kuvutia miradi mingi ya
maendeleo kama mradi wa maji wa Zumve uliotekelezwa na shirika la Water
for Good kwa kushirikiana na RUWASA, hatua itakayochochea ukuaji wa
uchumi na kuboresha maisha ya wananchi



0 Reviews