MZALE: AMANI NDIYO UTULIVU WA MAISHA YA KILA SIKU, TUSIIPOTEZE


Na Mwandishi Wetu

DAR ES SALAAM: AMANI imeelezwa kuwa ni msingi muhimu wa maisha ya kila siku, si tu kwa mtu binafsi bali pia kwa familia, jamii na taifa kwa ujumla. Hayo yamebainishwa na Waziri wa Mikopo wa Chuo cha Ardhi, Victor Mzale, ambaye anasisitiza kuwa amani huanza moyoni na huakisiwa katika namna watu wanavyoishi na kushirikiana.

Akizungumza kuhusu dhana ya amani, Mzale amesema kuwa amani ni utulivu wa moyo na nafsi, hali inayojenga mazingira ya kuaminiana na kushirikiana kwa ufanisi katika jamii. Ameeleza kuwa maelewano kati ya watu, iwe ni wazazi, vijana au jamii kwa ujumla, ndiyo chachu ya amani ya kweli.

“Pale ambapo kuna maelewano na watu wanapanga mambo yao kwa pamoja, ni rahisi kudumisha amani. Lakini pale maelewano yanapokosekana, hata mambo madogo yanaweza kuwa chanzo cha migogoro,” amesema.

Ameongeza kuwa Tanzania kwa sasa inaendelea kufurahia dira ya amani, lakini akatahadharisha kuwa tofauti za mitazamo zisichukuliwe kama sababu ya kuvunja amani. Badala yake, jamii inapaswa kujifunza kuvumiliana na kuheshimu mawazo tofauti bila kuleta mifarakano.

Kwa mujibu wa Mzale, kukosekana kwa maelewano ya pamoja kunaweza kuleta hofu hasa kwa vijana, kwani kunapunguza uhuru wa kupanga na kuchagua mustakabali wao. “Taifa lisipokuwa na mshikamano, vijana watakosa mwelekeo na matumaini ya kesho yao,” amesisitiza.

Aidha, ameonya kuwa amani inapopotea si rahisi kuirejesha kwa haraka. Mara nyingi, madhara yake huathiri nyanja mbalimbali za maisha, ikiwemo uchumi, elimu na ustawi wa jamii.

Akizungumzia mazingira ya vyuo na shule, Mzale amesema kuwa wanafunzi ni miongoni mwa makundi yanayoathirika zaidi pale amani inapovurugika. “Sisi tuliopo vyuoni tukikosa amani, tunahatarisha mustakabali wetu. Hatutakuwa na uwezo wa kufikia ndoto zetu,” amesema.

Kutokana na hilo, amependekeza kuwepo kwa vipindi maalum mashuleni vitakavyofundisha na kuhimiza umuhimu wa amani, ili kuijenga kwa vizazi vijavyo.

“Hakuna changamoto kubwa kama kuzoea kuishi kwa amani halafu ghafla ikaondoka. Ni hasara kubwa sana kwa mtu na taifa kwa ujumla,” amehitimisha

BOSS TV

Hii ni Official blog ya BOSS MEDIA kwa habari za siasa, jamii, elimu, burudani na michezo tufuatilie kwa uhakika zaidi

Post a Comment

Previous Post Next Post