TUMEPOTEZA ZAIDI YA MILIONI 221.7 KWA SABABU YA KUKOSA AMANI


MARA-TANZANIA: MENEJA Uendeshaji wa Kampuni ya Mafuta ya Nduuye, Isaya Manyata, mkazi wa Kanyama Isesa, Kata ya Bujora mkoani Mara, ameeleza masikitiko yake kufuatia hasara kubwa waliyoipata kutokana na matukio ya uvunjifu wa amani yaliyotokea Oktoba 29, 2025. Tukio hilo, amesema, linapaswa kuwa fundisho kwa Watanzania wote ili lisijirudie tena siku zijazo.

Akisimulia mkasa huo, Manyata amesema gari la kampuni yao lilikuwa likielekea katika kituo cha kushusha mafuta, lakini lilizuiwa njiani na kundi la vijana waliokuwa wamepanga mawe barabarani. Gafla, vijana hao walianza kufanya vurugu na kuharibu gari hilo pamoja na mali zilizokuwemo ndani yake, hali iliyosababisha hasara inayokadiriwa kufikia zaidi ya shilingi milioni 221.7.

“Tulipata hasara kubwa sana ambayo ingeweza kuepukika kama kungekuwa na amani. Hii ni pigo si kwa kampuni tu, bali pia kwa uchumi wa nchi kwa ujumla,” amesema Manyata kwa huzuni.

Ameongeza kuwa matukio hayo yanaonyesha wazi namna kukosekana kwa amani kunavyoweza kuathiri shughuli za kiuchumi na maisha ya watu wa kawaida. Kwa mujibu wake, hakuna maendeleo yanayoweza kupatikana katika mazingira ya vurugu na hofu.

Manyata ametoa wito kwa wananchi wote, hususan vijana, kujifunza kutokana na yaliyotokea na kuepuka kushiriki katika vitendo vinavyoweza kuvuruga amani ya nchi. Amesisitiza kuwa Tanzania haina nchi mbadala, hivyo ni jukumu la kila mmoja kulinda utulivu uliopo.

Aidha, amewahimiza wananchi wanaohisi kutosikilizwa na viongozi wao kuwa na subira na kufuata taratibu za kisheria katika kutatua changamoto zao. Amesema kuwa kufuata sheria na kanuni za nchi ni njia bora ya kufikia suluhisho la kudumu lenye kuzingatia amani na mshikamano.

“Ikitokea kuna jambo hujaridhika nalo, ni vyema kukimbilia mezani kwa mazungumzo na viongozi. Njia ya majadiliano huleta matokeo chanya zaidi kuliko kuchukua hatua za kiholela zinazoweza kusababisha madhara makubwa,” ameongeza.

Kwa kuhitimisha, Manyata amesisitiza umuhimu wa kuendeleza utamaduni wa mazungumzo, uvumilivu na kuheshimu sheria, akieleza kuwa hayo ndiyo msingi wa kudumisha amani na kuhakikisha maendeleo endelevu kwa taifa

BOSS TV

Hii ni Official blog ya BOSS MEDIA kwa habari za siasa, jamii, elimu, burudani na michezo tufuatilie kwa uhakika zaidi

Post a Comment

Previous Post Next Post