Read more
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan
ameainisha changamoto zinazopaswa kupewa kipaumbele ikiwemo kufungamanisha
ukuaji wa uchumi na sekta za uzalishaji.
Rais Samia amesema hayo kwenye maadhimisho ya miaka 62 ya Uhuru wa
Tanzania Bara sanjari na Mkutano wa kwanza wa uzinduzi wa Dira ya Taifa ya
Maendeleo 2050, yaliyofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete.
Aidha Rais Samia ametaka sekta mbalimbali za uzalishaji ziimarishwe zaidi ikiwemo
kilimo ambayo inakua kwa asilimia 4 tu kwa sasa tofauti na inavyotakiwa.
Pia amesisitiza kuimarishwa kwa ushiriki wa sekta binafsi ndani na nje ya nchi ili
kufanya wenyeji kuwa na utayari wa kupokea na kushirikiana na wageni wanaokuja
kuwekeza na kufanya biashara nchini.
Rais Samia amesema dira hiyo mpya itatakiwa kuzingatia kigezo cha kuongeza pato
la kila mwananchi kufikia dola za Kimarekani 3,000 kwa mwaka ambacho
hakikufikiwa katika dira ya mwaka 2000-2025.
Amesema kushindwa huko kulisababishwa na ukuaji wa uchumi kutojielekeza
kwenye sekta zinazogusa maisha ya watu wengi, hivyo umasikini vijijini haujapungua
kwa kasi iliyotarajiwa.
Kuhusu suala la Maadili ya Taifa (ethos), Rais Samia amesema ni muhimu taifa
kuwa na watu mahiri, makini na waadilifu ili kupata jamii inayochukia rushwa kila
mahali, inayojituma na kufanya kazi bila kusukumwa na inayopinga na kulaani
ukwepaji kodi.
Vile vile, Rais Samia ametoa wito kwa Watanzania wote ndani na nje ya nchi
(Diaspora) kushiriki kutoa maoni katika kuandaa Dira ya Taifa ya Maendeleo kupitia
njia za kisasa zitakazoainishwa na Tume ya Mipango.
Zuhura Yunus
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu



0 Reviews