Read more
Tanzania na Romania zimetia saini Hati mbili za makubaliano moja ikihusu kukuza
ushirikiano wa kiuchumi kisayansi na kiufundi katika sekta ya kilimo na mazingira.
Vile vile kumetiwa saini hati ya makubaliano kati ya Ofisi ya Waziri Mkuu na Wizara ya
Mambo ya Ndani ya Romania kwa ajili ya kushirikiana katika kukabiliana na maafa na
misaada ya kimataifa ya kibinadamu.
Utiaji saini huo umeshuhudiwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.
Samia Suluhu Hassan pamoja na Rais wa Romania nchini, Mhe. Klaus Werner Iohannis
ambaye yupo nchini kwa ziara ya Kitaifa.
Rais Samia, akizungumza na waandishi wa habari amesema Marais hao wawili
wamezungumzaia fursa zilizopo katika sekta za afya na utengenezaji wa dawa,
kubadilishana uzoefu katika sekta ya kilimo ikiwemo usindikaji wa mazao na kukabiliana
na majanga.
Aidha Rais Samia amesema mataifa hayo mawili yamekubaliana kuongeza wigo wa
ufadhili wa masomo hususan kwenye fani za udaktari na famasia ambapo Romania
imekubali kutoa nafasi kumi za masomo kwa Watanzania.
Wakati huo huo, Tanzania nayo imetoa nafasi tano za ufadhili kwa vijana wa Romania
kuja kusoma kwenye vyuo watakavyovichagua ikiwa ni fursa ya kuchangia jitihada za
Serikali za kujengea uwezo, rasilimali watu na kuimarisha huduma katika sekta
mbalimbali.
Akizungumzia mkutano wa Mabadiliko ya Tabianchi wa COP28, 2023 Rais Samia
amesema Tanzania inatarajia kuweka nguvu suala la nishati na nishati safi ya kupikia,
hivyo amemuomba Rais Iohannis kuiunga mkono Tanzania.
Rais Iohannis yupo nchini kwa ziara ya Kitaifa ya siku nne yenye lengo la kuimarisha
uhusiano baina ya nchi yake na Tanzania uliodumu kwa miaka 62 na ikiwa ni ziara ya
kwanza kwa Mkuu wa Nchi kutoka Jamhuri ya Romania kutembelea nchini.
Zuhura Yunus
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu



0 Reviews