Read more
NAIROBI, Kenya: WATU 14 wameuawa na wengine 17 kujeruhiwa katika kipindi cha Juni hadi Septemba mwaka huu, huku matukio ya uporaji na ujangili wa mifugo, Pamoja na migogoro kati ya jamii ikiendelea kusumbua maeneo ya Samburu, Meru na Isiolo nchini humo.
Matukio hayo yameendelea licha ya
serikali kuongeza operesheni za kiusalama katika maeneo yaliyoathirika.
Waziri wa Mambo ya Ndani wa Kenya,
Kipchumba Murkomen, aliiambia Kamati ya Bunge ya Taifa inayoshughulikia Utawala
na Usalama wa Ndani kwamba hali ya usalama kwa ujumla imeimarika katika maeneo
hayo.
Hata hivyo, alikiri kuwa ukosefu wa
usalama bado unaendelea kuwa tishio kwa maisha ya wananchi, shughuli za
kujipatia kipato na maendeleo ya kiuchumi.
“Kwa ujumla, hali ya usalama katika
maeneo yaliyoathirika imeimarika ikilinganishwa na vipindi vya nyuma,” alisema
Murkomen.
Licha ya maboresho hayo, serikali
inaendelea kukabiliwa na changamoto ya kudhibiti uhalifu unaohusisha wizi wa
mifugo, mashambulizi ya kulipiza kisasi na migogoro kati ya jamii, ambayo kwa
muda mrefu imekuwa ikiathiri baadhi ya maeneo ya kaskazini mwa Kenya.
Serikali imeendelea kuongeza
operesheni za kiusalama katika maeneo hayo kwa lengo la kuzuia mashambulizi
zaidi, kulinda maisha ya wananchi na kurejesha utulivu ili shughuli za kiuchumi
ziendelee bila hofu.

0 Reviews