Read more
JAB YAZINDUA RASMI MWONGOZO WA KISHERIA WA UTOAJI WA ITHIBATI YA

Bodi
ya Ithibati ya Waandishi wa Habari (JAB) imezindua rasmi Mwongozo wa
Kisheria wa Utoaji wa Ithibati ya Maisha kwa Waandishi wa Habari
Wakongwe, hatua inayolenga kutambua na kuthamini mchango wa waandishi wa
habari waliolitumikia Taifa kwa muda mrefu na kwa utumishi uliotukuka
katika maendeleo ya sekta ya habari nchini.
Uzinduzi
huo umefanyika leo, Julai 11, 2026, wakati wa maadhimisho ya JAB Day
yaliyofanyika katika Banda la Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na
Michezo kwenye Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam
(Sabasaba).
Kupitia hotuba yake iliyosomwa na
Dkt. Egbert Mkoko, Mwenyekiti wa Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa
Habari, Bw. Tido Mhando, alisema mwongozo huo umeandaliwa kwa kuzingatia
mamlaka iliyopewa Bodi chini ya Sheria ya Huduma za Habari, Sura ya 229
pamoja na Kanuni zake, ili kuweka utaratibu wa utoaji wa Ithibati ya
Maisha kwa waandishi wa habari wakongwe waliotoa mchango wa kipekee
katika maendeleo ya taaluma hiyo.
Alisema
mwongozo huo unawahusu waandishi wa habari ambao wakati Sheria ya Huduma
za Habari ilipoanza kutumika mwaka 2016 walikuwa na umri wa miaka 50 au
zaidi na walikuwa tayari wametoa mchango mkubwa katika sekta ya habari,
lakini hawakupata fursa ya kujiendeleza hadi kufikia sifa za kitaaluma
zinazohitajika kwa mujibu wa sheria.
"Mwongozo
huu unalenga kuhifadhi historia ya tasnia ya habari, kuthamini mchango
wa waandishi wa habari wakongwe na kuhakikisha uzoefu wao unaendelea
kuwa sehemu ya urithi wa taaluma ya uandishi wa habari nchini," ilieleza
sehemu ya hotuba ya Mwenyekiti.
Bw. Mhando
alisisitiza kuwa mwongozo huo hauondoi wala haupunguzi masharti ya
msingi yaliyowekwa na Sheria ya Huduma za Habari kuhusu sifa za kupata
ithibati kwa waandishi wa habari, bali unaweka utaratibu wa kutekeleza
mamlaka ambayo sheria imeipa Bodi kuhusu utoaji wa Ithibati ya Maisha
kwa watu wenye utumishi uliotukuka na waliotoa mchango wa kipekee katika
maendeleo ya sekta ya habari.
Aidha, aliipongeza Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa kuendelea kuiwezesha Bodi kutekeleza majukumu yake.
0 Reviews