Read more
Na Beda Msimbe, TBN, aliyekuwa Urusi
KWA miaka mingi, mazungumzo kuhusu nishati nchini Tanzania
yamekuwa yakitawaliwa na vyanzo vya maji, gesi asilia, na sasa nishati jadidifu
kama jua na upepo.
Hata hivyo, kauli ya hivi karibuni ya Rais Samia Suluhu
Hassan akiwa nchini Urusi imethibitisha kuwa Tanzania sasa imedhamiria kuingia
kwenye Klabu ya Nyuklia ifikapo mwaka 2029.
Hili si jambo la kubahatisha bali ni mkakati unaoendeshwa na
uwepo wa akiba kubwa ya madini ya urani katika Bonde la Mto Mkuju mkoani
Ruvuma, mradi unaosubiriwa kwa hamu kubwa kuwezesha fursa ya maendeleo. Mkakati
huu unalenga kuipa nchi vyanzo mbadala na imara vya nishati ili kukabiliana na
changamoto za kukatika kwa umeme na kukua kwa kasi kwa sekta ya viwanda.
Historia ya mradi wa urani wa Mkuju River uliopo ndani ya
mfumo wa ikolojia wa Selous na Nyerere kusini mwa Tanzania inaonyesha kuwa
unatajwa kuwa miongoni mwa hifadhi kubwa zaidi za urani ambazo hazijachimbwa
duniani kote.
Mradi huu unamilikiwa na kampuni ya Mantra Tanzania, ambayo
ni kampuni tanzu ya Uranium One inayomilikiwa na Shirika la Nishati la Atomiki
la Urusi liitwalo Rosatom.
Ugunduzi wa madini haya ulileta matumaini makubwa tangu
miaka ya 2010 ambapo tafiti za kijiolojia zilionyesha kuwa eneo hilo lina
hifadhi inayokadiriwa kufikia tani milioni 152 za miamba yenye madini hayo
inayoweza kuzalisha mamilioni ya ratili za urani iliyosafishwa kwa kiasi fulani
kwa miaka zaidi ya 12 hadi 20 ya uhai wa mgodi huo.
Hata hivyo, mradi huo ulikabiliwa na changamoto mbalimbali
zilizosababisha usitishwaji wa muda ikiwemo kuanguka kwa bei ya urani duniani
baada ya ajali ya nyuklia ya Fukushima nchini Japani mwaka 2011.
Mahitaji ya urani duniani yalishuka sana na kupelekea bei
kuporomoka hali iliyofanya uchimbaji wa Mkuju kutokuwa na tija ya kibiashara
kwa wakati huo.
Changamoto nyingine ilikuwa ni mazingira na udhibiti kwa
kuwa eneo la mradi lilikuwa ndani ya Hifadhi ya Selous ambayo ni eneo la Urithi
wa Dunia, jambo lililolazimisha serikali kufanya mabadiliko ya mipaka ili
kuruhusu uchimbaji bila kuathiri ikolojia nzima ya eneo hilo.
Baada ya usingizi wa muda mrefu, mradi wa Mkuju sasa
unafufuka kwa kasi kubwa kutokana na kupanda upya kwa bei ya urani duniani na
msukumo wa kisiasa kutoka kwa serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia
Suluhu Hassan.
Kwa sasa, Mantra Tanzania na Uranium One wamekamilisha hatua
za majaribio ya teknolojia ya uchenjuaji iitwayo In-Situ Recovery au majaribio
ya kinu cha majaribio.
Teknolojia hii ni ya kisasa na salama zaidi kimazingira
kwani haihusishi kuchimba mashimo makubwa bali huingiza vimiminika maalum
ardhini vinavyoyeyusha urani na kuivuta juu ikiwa kimiminika.
Mazingira ya sasa yanaonyesha kuwa miundombinu ya msingi
ikiwemo barabara za kuingia eneo la mradi, mifumo ya ulinzi wa mionzi, na kambi
za wafanyakazi zimeshaimarishwa huku serikali kupitia Tume ya Nguvu za Atomiki
Tanzania ikifanya ukaguzi wa mara kwa mara ili kuhakikisha usalama wa mionzi
unazingatiwa kabla ya uchimbaji kuanza kikamilifu.
Ukimya wa miaka kadhaa uliacha maswali mengi lakini sasa
wananchi na wadau wa kiuchumi wanasubiri kwa shauku kubwa kuanza kwa mgodi huu
kwa sababu ya fursa za ajira na uchumi wa ndani.
Wakazi wa mikoa ya Kusini hasa Ruvuma na Lindi wanatarajia
fursa za ajira za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja pamoja na kukuza
biashara za ndani kupitia usambazaji wa bidhaa mgodini.
Mradi huu pia unatajwa kuwa chanzo kipya na kikubwa cha
mrabaha na kodi kwa serikali utakaosaidia kufadhili miradi mingine ya kijamii
kama afya na elimu huku kukiwa na matumaini ya uhuru wa nishati kwani kauli ya
Rais Samia kuwa urani hii itatumiwa kuzalisha umeme nchini inaleta matumaini
mapya kuwa Tanzania haitakuwa tu msafirishaji wa mali ghafi bali itakuwa
mtumiaji wa mwisho wa teknolojia hiyo.
Uthibitisho mkubwa zaidi unaoonyesha kuwa Tanzania inaenda
kuwa na kinu cha nyuklia kwa siri na umakini mkubwa ni kuwepo kwa mkataba wa
faragha ambao unazuia pande mbili yaani Shirika la Umeme Tanzania na Shirika la
Rosatom la Urusi kusema chochote wakati wa mazungumzo mpaka yafikie mwisho.
Wataalamu wa sekta ya nishati na sheria nchini wameeleza
kuwa mkataba huu wa kisheria wa kutosambaza taarifa ni wa kawaida lakini wa
kiwango cha juu sana unapohusisha masuala nyeti ya usalama na nishati ya
kimkakati kama nyuklia.
Siri hii kubwa inalinda maslahi ya taifa na kuzuia
kuingiliwa kati kwa mazungumzo hayo na mataifa mengine au washindani wa
kijiografia kabla ya makubaliano kamili kukamilika.
Hatua hii ya usiri inatafsiriwa na wachambuzi kama ishara ya
wazi kwamba pande zote mbili ziko katika hatua za mwisho za kiufundi na
kisheria kufanikisha ujenzi wa kinu hicho bila kuleta taharuki.
Ili kufikia maono ya mwaka 2029 ya kuwa na kinu cha nyuklia,
Tanzania inakabiliwa na kibarua kizito cha kujenga udhibiti madhubuti wa
kisheria na kitaalamu.
Rais Samia akizungumza na waandishi wa habari mjini St
Petersburg, Urusi wakati akihudhuria Jukwaa la Uchumi la Kimataifa la
Petersburg, alibainisha kuwa Tume ya Nguvu za Atomiki Tanzania sasa itakuwa na
kazi kubwa inayohusiana na masuala ya matumizi ya nyuklia kwa amani kama
inavyoelekezwa na Shirika la Kimataifa la Nguvu za Atomiki.
Ushirikiano mpya na Urusi hautalenga tu kununua mitambo bali
kuhamisha teknolojia kwa kutoa mafunzo ya wahandisi wa kiasili yanayofadhiliwa
kwa sasa nchini Urusi, jambo ambalo ni la msingi sana kwani usalama wa kinu cha
nyuklia unategemea kwa asilimia mia moja uwezo, maarifa, na umakini wa wanadamu
wanaokiongoza.
Wataalamu wa nishati kutoka serikalini wanasisitiza kuwa
hatua hii ya sasa ya kimkakati itaiwezesha nchi kuwa na uhakika kamili wa
nishati ya viwanda ambayo haitayumba kutokana na mabadiliko ya tabianchi kama
ilivyo kwa nishati ya maji.
Kauli za wataalamu hao zilianikizwa na Rais Samia Suluhu
Hassan aliyesema jwamba ni lengo la serikali kuwa na taifa ambalo linazalisha
jumla ya megawati 8000 ili kuwa na ziada ya uhakika ya kuuza nchi za nje.
Mazungumzo yanayoendelea chini ya mkataba wa faragha
yanalenga kuhakikisha kuwa ujenzi wa kinu hicho unazingatia viwango vyote vya
kimataifa na gharama zinazohimilika kwa uchumi wa Tanzania.
Hii inaonyesha kuwa serikali haikurupuki bali inasonga mbele
kwa hatua madhubuti zilizofanyiwa utafiti wa kina ili kulinda maslahi ya kizazi
cha sasa na kijacho.
Safari ya kuelekea mwaka 2029 imeshaanza kwa kasi kubwa na
ya kimyakimya chini ya usimamizi thabiti Rais Samia Suluhu Hassan ambapo ziara
yake nchini Urusi pamoja na kuwa na mafanikio makubwa kisiasa na kiuchumi,
imewezesha kuwepo kwa mikataba ya makubaliano kadha yanayogusa teknolojia ya
nyukilia.
Urani ya Mkuju si hadithi tena ya madini yaliyolala ardhini
bali ni mtaji wa kimkakati unaokwenda kubadilisha kabisa ramani ya nishati
katika ukanda mzima wa Afrika Mashariki na Kati.
Kama ahadi ya Rais Samia itatimizwa na mazungumzo ya siri
yaliyopo sasa yakazaa matunda yaliyokusudiwa, ifikapo mwaka 2029 moshi na
mwanga kutoka kwenye kinu cha kwanza cha nyuklia cha Tanzania utakuwa ndio
ushahidi tosha wa nchi iliyoamua kuikumbatia nishati ya kesho kwa ajili ya
maendeleo endelevu ya leo.



0 Reviews