Read more
DODOMA: MBUNGE wa Jimbo la Musoma Mjini, Mgore Kigera, amewataka Watanzania kuendelea kuipenda nchi yao na kushiriki kikamilifu katika kulinda amani ambayo imeendelea kuwa nguzo muhimu ya maendeleo ya taifa.
Kigera amesema Tanzania imebarikiwa kuwa na mazingira ya amani na utulivu ambayo yamewezesha wananchi kufanya shughuli zao za kila siku kwa uhuru na kuendelea kuchangia ukuaji wa uchumi wa nchi.
Akizungumza kuhusu umuhimu wa amani, mbunge huyo alieleza kuwa maendeleo hayawezi kupatikana katika mazingira yenye migogoro na kutokuelewana. Alisema amani ndiyo msingi wa mafanikio katika ngazi zote za maisha kuanzia familia hadi taifa.
Kwa mujibu wa Kigera, amani huanza kujengwa ndani ya familia kabla ya kuonekana katika jamii na taifa kwa ujumla. Alifafanua kuwa familia isiyokuwa na maelewano haiwezi kufikia malengo yake wala kuishi kwa utulivu.
“Katika maisha siyo tu kwa Watanzania, hata sisi kwenye familia zetu, ukiwa mama, baba ama watoto, kukiwa hakuna amani ndani ya nyumba hakuna kitakachoendelea,” amesema Kigera.
Amesema kauli hiyo inapaswa kuwa funzo kwa kila mwananchi kutambua kuwa amani si jukumu la serikali pekee, bali ni wajibu wa kila mmoja kuanzia katika mazingira yake ya karibu.
Mbunge huyo amesisitiza kuwa wazazi wanapaswa kuwa mfano wa kuigwa katika malezi ya watoto kwa kuwafundisha misingi ya heshima, uvumilivu na mshikamano ambayo huchangia kujenga jamii yenye amani.
Aidha, amewahimiza vijana kutumia nguvu na ubunifu wao katika shughuli za maendeleo badala ya kujiingiza katika vitendo vinavyoweza kuhatarisha utulivu wa jamii.
Kigera pia amewataka viongozi wa ngazi mbalimbali kuendelea kuwa mstari wa mbele katika kuhubiri umoja na mshikamano miongoni mwa wananchi ili kuimarisha zaidi misingi ya amani iliyopo nchini.
Amehitimisha kwa kusisitiza kuwa Tanzania itaendelea kupiga hatua kubwa za maendeleo ikiwa wananchi wote wataungana katika kulinda amani na kudumisha mshikamano uliopo kwa manufaa ya vizazi vya sasa na vijavyo.



0 Reviews