Read more
Filamu ya uchunguzi iliyotengenezwa na mwanahabari wa uchunguzi kutoka Nigeria anayeishi Ghana, David Hundeyin, imezua mjadala mpana kuhusu nafasi ya vijana, wajibu wa vyombo vya habari na umuhimu wa kulinda amani na utulivu katika jamii za Afrika.
Akizungumza
baada ya kuonyeshwa kwa filamu hiyo, Waziri wa zamani wa Afya Zanzibar
na mwanasiasa mkongwe, Hamad Rashid, amesema kazi hiyo imefungua macho
ya wananchi kuhusu namna matukio makubwa ya kijamii na kisiasa
yanavyoweza kuathiriwa na nguvu za nje. Amesisitiza umuhimu wa Waafrika
kujenga uwezo wa kufanya tafiti na uchunguzi wa kina kuhusu masuala
yanayowahusu.
Amesema pamoja na filamu hiyo
kutoa mafunzo muhimu kwa jamii, hatua inayopaswa kuchukuliwa sasa ni
kutumia yaliyobainishwa kama somo la kujenga taifa lenye amani, umoja na
maendeleo badala ya kuendeleza migawanyiko.
"Changamoto
kubwa zinazowakabili wananchi ni ajira, afya, elimu na ustawi wa
maisha. Nguvu kubwa inapaswa kuelekezwa katika kutatua mahitaji hayo kwa
manufaa ya jamii na taifa kwa ujumla," amesema Hamad Rashid.
Kwa upande wake, mwanazuoni na mchambuzi wa masuala ya maendeleo
kutoka Zimbabwe, Joshua Maponga, amesema filamu hiyo imeonesha umuhimu
wa vyombo vya habari vya ndani kuwa na uwezo wa kuripoti kwa kina
masuala yanayotokea katika jamii zao ili kutoa taswira halisi kabla
simulizi za nje hazijatawala mjadala.
Ameongeza
kuwa vijana wanapaswa kuwa waangalifu dhidi ya ushawishi unaoweza
kuwaingiza katika migogoro inayoweza kuhatarisha mustakabali wao na
maendeleo ya nchi zao. Amesema nguvu za vijana zinapaswa kuelekezwa
katika ubunifu, uzalishaji na ujenzi wa uchumi badala ya kushiriki
katika matukio yanayoweza kuhatarisha amani na utulivu.
Akielezea sababu za kuandaa filamu hiyo, David Hundeyin amesema
lengo kuu lilikuwa kuonesha namna ushawishi wa nje unavyoweza kujitokeza
katika jamii za Afrika kupitia njia mbalimbali, ikiwemo mitandao ya
kijamii na mashirika yenye maslahi ya kisiasa au kiuchumi.
Amesema
Waafrika wengi bado hawatambui kwa kiwango kikubwa namna masuala ya
kimataifa yanavyoweza kuathiri maisha yao ya kila siku, hivyo aliona
umuhimu wa kutumia filamu hiyo kama mfano wa kuhamasisha uelewa mpana
kuhusu athari za siasa na maslahi ya kimataifa katika maendeleo ya bara
la Afrika.



0 Reviews