Na OWM KAM - Njombe
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi kwenye maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani itakayofanyika kitaifa mkoani Njombe tarehe moja Mei mwaka huu.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu - Kazi, Ajira na Mahusiano, Mhe. Deus Sangu, ametoa taarifa hiyo leo Aprili 29, 2026, mjini Njombe, akisema Rais amekubali mwaliko huo na wananchi pamoja na wafanyakazi wanatarajiwa kujitokeza kwa wingi.
“Kupitia kwenu napenda kuwataarifu kuwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan atakuwa mgeni rasmi kwenye maadhimisho ya Mei Mosi mwaka huu hapa mkoani Njombe. Hii ni fursa kubwa kwa wananchi wa Njombe kuonana na Rais tangu tulipokamilisha uchaguzi mkuu wa mwaka 2025,” alisema Waziri Sangu.
Maadhimisho hayo yatafanyika katika Uwanja wa Halmashauri ya Mji Njombe, chini ya kauli mbiu isemayo: “Kazi Zenye Staha ni Nguzo Imara kwa Maendeleo Endelevu katika Utekelezaji wa Dira ya Taifa 2050”.
Katika hatua nyingine, Waziri Sangu aliwataka waajiri nchini kutekeleza sheria za kazi, ikiwemo kuhakikisha watumishi wao wanapata mikataba ya kazi, hatua itakayosaidia wafanyakazi kupata michango kwenye mifuko ya hifadhi ya jamii.
“Kijana anapokosa mkataba inapelekea pia akose haki yake ya kuchangia kwenye mifuko ya hifadhi ya jamii kama NSSF na WCF hivyo kumkosesha mafao ya uzeeni. Serikali itaendelea kuchukua hatua kali dhidi ya waajiri wasiotoa mikataba kwa wafanyakazi wao,” alisisitiza Waziri Sangu.
Kuhusu hatua za utekelezaji, Waziri Sangu amemwagiza Kamishna Kazi kuongeza kasi kwenye ukaguzi wa sheria za kazi ili waajiri waweze kutekeleza kwa ukamilifu na watumishi wapate stahiki zao.
Waziri Sangu alikagua pia mabanda ya maonesho kwenye uwanja wa Shule ya Msingi Mji Mwema Njombe, akipongeza Wakala wa Usalama na Afya Mahala pa Kazi (OSHA) kwa uratibu wa maonesho hayo ambapo zaidi ya taasisi binafsi na za umma 200 zimeshiriki.
