WATANZANIA wanapaswa kuelewa kuwa mwanzo wa kuponya majeraha ya taifa letu ni kuacha kusikiliza kelele na upotoshaji unaosambazwa mitandaoni na badala yake kutumia akili na utafiti kujua ukweli ulioibuliwa na Tume ya Jaji Mohamed Chande.
Ukifuatilia maonio mtandaoni utabaini kwamba washiriki wengi wanaona haja ya mshikamano wa kitaifa.
Wengi wao wanasema ili kuendeleza taifa, Watanzania wanapaswa kutumia ripoti hii kama mwongozo wa kudai uwajibikaji na si kuipuuza kwa mihemko ya kisiasa ya mitandaoni.
Ukweli uliowekwa na Jaji Chande ndio mwanzo wa mchakato wa kisheria utakaofikisha wahalifu mahakamani, kuwepo kwa mabadiliko ya Katiba na mfumo wa uchaguzi.
Kujielimisha na kuuelewa ukweli huu mchungu ndiyo njia pekee ya kutumia elimu yetu kwa faida ya wote na kuhakikisha kuwa damu ya Watanzania haimwagiki tena kwa uzembe wa viongozi au vyombo vya dola.
Ingawa kuna watu wanadai mitandaoni kuwa ripoti hii ni mbinu ya kuisafisha Serikali, ukweli ni kwamba Jaji Chande amepasua jipu kwa kuibua vyanzo vya ghasia za Oktoba 2025. Hivyo kuendelea kuipuuza kazi hii kama sifuri ni kujinyima fursa ya kuleta mabadiliko ya kimfumo yanayohitajika ili kuzuia maafa kama hayo yasitokee tena huko mbeleni.
Uchambuzi wa kina wa ripoti hiyo unaonyesha kuwa Serikali imetamkwa kwa asilimia kubwa ya kuwa chanzo cha ghasia kwa kutotatua kero za muda mrefu za wananchi. Tume imeweka wazi kuhusu madai ya Katiba mpya, kero za kodi, rushwa, na utendaji mbovu wa watumishi wa umma.
Vilevile Tume imebainisha kuwa mivutano ya ndani ya vyama wakati wa uteuzi wa wagombea ilikuwa kichocheo kikubwa cha vurugu. Kwa kuwa CHADEMA haikushiriki uchaguzi huo, lawama za kukatana majina ambazo Tume imezisema zinalenga moja kwa moja vikao vya juu vya Chama Cha Mapinduzi vilivyowakata washindi wa kura za maoni na kuibua ghasia kama zile zilizotokea Tanga Mjini. Hii inathibitisha kuwa Jaji Chande hajaacha upande wowote salama, bali ameweka ukweli mezani kuhusu jinsi uroho wa madaraka unavyotishia amani ya nchi.
Kuhusu vyombo vya ulinzi na usalama, ripoti imeviaibisha kwa kuonyesha jinsi vilivyolala usingizi wa pono huku viashiria vya ghasia vikiwa wazi miezi sita kabla. Ni jambo la kushtua na kusikitisha kusikia kuwa vijana zaidi ya mia tano walikuwa wakipewa mafunzo ya vurugu kwenye makambi yaliyopo mita chache kutoka vituo vya polisi lakini vyombo vyetu vikasema vimeshtukizwa. Hapa Jaji Chande ameweka wazi kuwa kulikuwa na uzembe wa hali ya juu na utendaji wa mazoea ambao umeligharimu taifa maisha ya watu na mali zao.
Jambo la ujasiri zaidi lililofanywa na Jaji Chande ni kuthibitisha kuwa kulikuwa na matumizi haramu ya silaha na ukatili dhidi ya raia wasio na hatia. Mifano ya kusikitisha ya mtoto aliyepigwa risasi ya kichwa akiwa mgongoni mwa mama yake na mauaji ya watu kumi na tatu kwenye banda la kuonyeshea picha ni kielelezo tosha kuwa Tume haikusafisha jeshi la polisi. Badala yake, imetaka kila askari aliyehusika kuwajibika binaf