Read more
SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar imewatoa hofu Mfuko wa
Hifadhi ya Huduma za Jamii Zanzibar, (ZSSF) na kuwataka
kuwekeza fedha zao kwenye miradi mikubwa ya Serikali ya
kimakakati.
Pia, Serikali imejizatiti kuweka dhamana ya miradi mikubwa ya
maendeleo itakayotekelezwa na Mfuko huo pamoja na kuwahakikishia
usalama wa fedha zao endapo zitaathiriwa kwa namna yoyote na
ujenzi wa miradi hiyo.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein
Ali Mwinyi, aliyasema hayo alipoweka jiwe la msingi la ujenzi wa
maegesho ya magari, Malindi Wilaya ya mjini, Mkoa wa Mjini
Magharibi.
Alisema, lengo la Serikali kuweka ujenzi wa maegesho hayo ni
kupunguza msongamano wa magari mjini pamoja na kuweka usafiri
wa umma wa aina moja na wa kisasa ili kwenda sambamba na
mahitaji ya mji kwa wakati uliopo.
Alisema, hayo ni maegesho ya kwanza ya ghorofa kujengwa Zanzibar,
yenye hadhi na mitambo ya kisasa.
Rais Dk. Mwinyi alitoa ushuhuda wa Mifuko ya hifadhi ya Jamii kwa
mataifa mengine duniani ikiwemo Indoneia na Malaysia yamejenga
nchi zao kwa kuweka miundominu ya kisasa, miji mikubwa, maduka,
barabara na madaraja makubwa ya maendeleo, hivyo aliwatoa
wasiwasi ZSSF na kuwataka kuiga mifano ya mataifa hayo kwa
kuijenga upya Zanzibar bila kujali hasara ya fedha zao kwani Serikali
imewapa dhamana ya fedha hizo.
Alisema, Serikali pia imepanga kuweka vituo vikuu viwili vya mabasi
ya umma kwa maeneo ya Kijangwani na Malindi ili kukidhi hadhi ya mji
yenye kwenda sambamba na maendeleo ya mataifa mengine duniani.
Akizungumzia athari zinazoathiri Hifadhi ya Taifa ya Mji MKongwe wa
Zanzibar, Rais Dk. Mwinyi amesema ujenzi wa maegesho hayo
umezingatia na kufuata taratibu zote zilizowekwa na hifadhi hiyo kwa
mujibu wa matakwa ya UNESCO juu ya mabadiliko ya maendeleo
yanayotekelezwa kwenye maeneo ya Mji Mkongwe.
Aidha, Dk. Mwinyi alieleza, maegesho hayo yatapunguza
msongamano maeneo ya Darajani na Mji Mkongwe kwa kutoruhusu
baadhi ya vyombo vya usafiri kuingia kwenye hifadhi ya mji Mkongwe
ili kuunusuru mji huo na athari ya vyombo hivyo.
Akizungumzia athari kwa Hifadhi ya Taifa ya Mji MKongwe wa
Zanzibar, Rais Dk. Mwinyi amesema ujenzi wa maegesho hayo
umezingatia na kufuata taratibu zote zilizowekwa na hifadhi hiyo kwa
mujibu wa matakwa ya UNESCO.
Kuhusu mazingira ya wafanyabiashara wa maeneo ya mjini (Darajani),
Dk. Mwinyi alieleza Serikali imekusudia kujenga eneo maalumu la
wafanyabiashara hao lenye hadhi ya juu na mwonekano wa kisasa, ili
kuepusha wafanyabiashara kuenea kiholela barabarani na kueleza
kuwa eneo la Darajani ni kitovu kikuu cha biashara, Zanzibar.
Alisema, ujenzi huo pia utahusisha barabara kuu ya Darajani pamoja
na eneo maalum la wafanyabiasha.
Naye Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa
na Idara Maalum za SMZ, Masoud Ali Mohammed, alisema juhudi za
Mapinduzi zinazoendelezwa na awamu ya nane ya Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar ni mapinduzi ya Uchumi na kuboreshwa
maendeleo kwa kuendelezwa miradi mikubwa ya maendeleo kwenye
sekta zote za jamii ikiwemo Afya, elimu, sekta ya miundombinu na
Barabara, maji safi, makaazi ya kisasa ya wananchi na viwanja vya
michezo vyenye hadhi ya kimataifa.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Aboud Hassan
Mwinyi, alisema ujenzi wa maegesho hayo unatarajiwa kuchukua gari
200 kwa wakati mmoja, utagharimu bilioni 6.83 hadi kukamilika kwake
na sasa umefikia asilimia 65 ya ujenzi wote.
Pia, alisema ujenzi huo umetoa ajira kwa wazawa ikiwemo
wakandarasi wasaidizi pamoja na Serikali kukusanya mapato
yanayotokana na ujenzi huo.
Mapema akizungumza kwenye hafla hiyo, Mkurugenzi Mwendeshaji
wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar (ZSSF), Nassor Shaaban
Ameir alisema mbali na mradi huo wa maegesho ya magari ya ghorofa
Malindi, pia wanatarajia kuanza ujenzi mwengine wa kituo kikubwa
cha mabasi ya uma kwenye eneo hilo.
IDARA YA MAWASILINO, IKULU ZANZIBAR


0 Reviews