DKT. MWIGULU AAGIZA UFANYIKE UCHUNGUZI WA KUSHUKA KWA BEI YA MIWA

DKT. MWIGULU AAGIZA UFANYIKE UCHUNGUZI WA KUSHUKA KWA BEI YA MIWA

Size
Price:

Read more

 


▪ Bodi ya Sukari itume wataalamu kubaini chanzo cha tatizo

▪ Aagiza kuchunguzwa kwa malalamiko dhidi ya uongozi wa Kijiji cha Iwemba

WAZIRI MKUU, Dkt. Mwigulu Nchemba, ameiagiza Bodi ya Sukari Tanzania itume timu ya wataalamu kuchunguza sababu za kushuka kwa bei ya miwa inayouzwa na wakulima wa Mikumi, mkoani Morogoro.

Dkt. Mwigulu ametoa agizo hilo leo, Jumatatu, Novemba 23, 2026, wakati akizungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye viwanja vya Shule ya Sekondari Mikumi Day, Mji Mdogo wa Mikumi, Wilaya ya Kilosa, mkoani Morogoro, kufuatia malalamiko ya wakulima kuhusu bei hiyo na madai ya kuwapo kwa vitendo visivyo vya uaminifu katika biashara ya zao hilo.

Amesema anatambua kuwa bei ya miwa inaweza kupanda au kushuka kutokana na mwenendo wa soko, lakini wakati mwingine mabadiliko hayo yanaweza kuchangiwa na vitendo visivyo vya uaminifu. “Wakati mwingine ni soko, lakini wakati mwingine huwa zinakuwepo na janja janja. Na hata sasa nimegusiwa kwamba zipo na janja janja,” amesema.

Waziri Mkuu ameiagiza Bodi ya Sukari, kwa kushirikiana na Wizara ya Kilimo, kutuma wataalamu watakaokutana na vyama vya ushirika na wakulima ili kubaini chanzo halisi cha tatizo hilo. “Sasa nielekeze Bodi ya Sukari itume wataalamu waje waonane na vyama vya ushirika pamoja na nyinyi wenyewe wakulima, ili tujue mzizi hasa wa tatizo,” amesema.

Aidha, ameagiza taarifa ya uchunguzi huo iwasilishwe kwake moja kwa moja ili aweze kutoa maelekezo kuhusu hatua zinazopaswa kuchukuliwa kuhakikisha wakulima wananufaika na shughuli zao za uzalishaji.


“Na taarifa hiyo niipate mwenyewe ili niweze kuelekeza hatua stahiki za kuchukua, ili tuweze kuhakikisha jasho la wakulima wa miwa linapata faida kutokana na nguvu anayowekeza katika kulima,” amesema.

Awali, Mbunge wa Mikumi ambaye pia ni Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Denis Lazaro Londo, alimweleza Waziri Mkuu kuwa licha ya uwekezaji wa zaidi ya Sh. bilioni 300 katika upanuzi wa Kiwanda cha Sukari cha Kilombero, wakulima bado wanakabiliwa na changamoto ya kushuka kwa bei ya miwa.

Amesema kilimo cha miwa ni miongoni mwa shughuli muhimu za kiuchumi katika eneo hilo na kwamba kushuka kwa bei kunapunguza mapato ya wakulima.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu ameagiza kufanyika kwa uchunguzi wa malalamiko dhidi ya uongozi wa Kijiji cha Iwemba, Kata ya Kidodi, Tarafa ya Mikumi, Wilaya ya Kilosa, na kuelekeza hatua zichukuliwe endapo itathibitika kuwa viongozi hao wamekiuka sheria au kutumia vibaya madaraka yao.

Amemwelekeza Mkuu wa Wilaya ya Kilosa kwenda katika kijiji hicho, kuitisha mkutano wa hadhara na kuwasikiliza wananchi ili kubaini ukweli wa malalamiko yaliyowasilishwa. “Mkuu wa Wilaya, tumeshamaliza ziara, nenda pale pale itisha mkutano wa hadhara, kawasikilize wale wananchi wote pale,” amesema.

Dkt. Mwigulu pia amemtaka Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Queen Sendiga, ahakikishe hatua stahiki zinachukuliwa kwa mujibu wa sheria na taratibu dhidi ya viongozi watakaobainika kukiuka wajibu wao, wakiwemo viongozi waliochaguliwa na watumishi walioajiriwa.


“Pakithibitika pana ukiukwaji wa matumizi ya ofisi, Mkuu wa Mkoa futa uongozi wote pale. Na wa kuajiriwa waachishwe kazi,” amesema.

Hata hivyo, amesisitiza umuhimu wa uchunguzi wa haki ili kuhakikisha hakuna anayechukuliwa hatua bila kuthibitishwa kwa tuhuma zinazomkabili. “Nenda ukasikilize, pata undani, na wala hatutaki kuonea mtu. Lakini hatuwezi tukalea uzembe,” amesema.

Awali, Naibu Waziri katika Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI, Dkt. Festo Dugange, alisema zaidi ya barua saba za malalamiko dhidi ya mwenyekiti na mtendaji wa Kijiji cha Iwemba zimewasilishwa, zikihusu namna viongozi hao wanavyotekeleza majukumu yao.

0 Reviews

Contact form

Name

Email *

Message *