Read more
WAZIRI Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba, leo Julai 7, 2026, amewasili katika Makao Makuu ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) yaliyopo jijini Paris, Ufaransa, kwa ajili ya kumwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan kwenye Maadhimisho ya Tano ya Siku ya Kiswahili Duniani.
Dkt. Mwigulu alipowasili katika makao makuu ya UNESCO alipokelewa na Mkurugenzi Mkuu wa shirika hilo, Khaled El-Enany, ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya maadhimisho hayo yanayolenga kuenzi na kuendeleza lugha ya Kiswahili duniani.
Maadhimisho ya Siku ya Kiswahili Duniani yameendelea kuwa jukwaa muhimu la kutambua mchango wa lugha hiyo katika kuimarisha utamaduni, elimu, diplomasia na mshikamano wa watu katika mataifa mbalimbali, huku yakihusisha viongozi, wataalamu wa lugha na wadau kutoka sehemu tofauti za dunia.
Ushiriki wa Tanzania katika maadhimisho hayo unaendelea kuonyesha nafasi ya nchi katika kukuza na kuhifadhi Kiswahili, lugha ambayo imeendelea kupata hadhi na kutambuliwa kimataifa kutokana na mchango wake katika mawasiliano na maendeleo ya jamii.
Maadhimisho ya mwaka huu yanatarajiwa kuangazia fursa za kuendelea kukiendeleza Kiswahili katika nyanja mbalimbali ikiwemo elimu, sayansi, teknolojia na utamaduni, sambamba na kuimarisha ushirikiano wa kimataifa katika kukieneza na kukitumia lugha hiyo duniani.

0 Reviews