Read more
Wahadzabe hao, waliowasili kutoka Mkoa wa Arusha,
walipata fursa ya kuonesha baadhi ya mila, desturi na mbinu zao za maisha ya
asili, hali iliyowavutia washiriki wengi wa tamasha hilo kutoka ndani na nje ya
Tanzania. Wageni walionekana kuwa na hamu kubwa ya kujifunza kuhusu historia,
maisha na utamaduni wa jamii hiyo maarufu kwa maisha ya uwindaji na ukusanyaji.
Akizungumza katika tamasha hilo, Waziri wa Nchi,
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hamza Hassan Juma, alisema uwepo
wa Wahadzabe ni sehemu ya utalii wa kiutamaduni unaoifanya Zanzibar kuwa kitovu
cha kukutanisha watu wa tamaduni mbalimbali kutoka Tanzania na duniani kote.
Alisema tamasha la ZIFF limeendelea kuwa jukwaa
muhimu la kuonesha utofauti wa tamaduni zilizopo nchini, huku likiwapa wageni
nafasi ya kujifunza na kuthamini urithi wa makabila mbalimbali ya Tanzania.
Aidha, aliipongeza ZIFF kwa kuendelea kutumia sanaa na filamu kama nyenzo ya
kuimarisha umoja na kuitangaza Tanzania kimataifa.
Washiriki wengi waliohudhuria tamasha hilo
walieleza kufurahishwa na uwepo wa Wahadzabe, wakisema umetoa sura tofauti na
ya kipekee katika ZIFF 2026. Wengi walitumia fursa hiyo kujifunza kuhusu maisha
yao ya jadi, jambo lililoifanya jamii hiyo kuwa miongoni mwa vivutio vikubwa
vya tamasha la mwaka huu.
0 Reviews