Read more
Mkuu wa Wilaya ya Ulanga, Khamana Juma Simba, amewataka vijana wa wilaya hiyo kuwa mstari wa mbele katika kulinda amani ya taifa ili kuwezesha wananchi kufanya shughuli zao za maendeleo kwa uhuru na utulivu. Amesema amani ndiyo msingi wa maendeleo endelevu, hivyo kila kijana anapaswa kushiriki kikamilifu katika kuilinda na kuitunza kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.
Simba alitoa kauli hiyo wakati wa uzinduzi wa Jukwaa la Vijana (Youth Platform), linalolenga kuwakutanisha vijana kwa ajili ya kujadili masuala mbalimbali ya maendeleo, fursa za kiuchumi na namna ya kushiriki katika shughuli za kujiletea maendeleo binafsi na ya jamii kwa ujumla.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mkuu huyo wa Wilaya alisema vijana wanapaswa kuwa walinzi wa amani katika jamii zao kwa kuchangia kupunguza vitendo na tabia zinazoweza kuhatarisha utulivu wa nchi. Alisisitiza kuwa maendeleo ya kweli hayawezi kupatikana katika mazingira yenye migogoro au vurugu, hivyo jukumu la kulinda amani linawahusu wananchi wote, hususan vijana ambao ndiyo nguvu kazi ya taifa.
Pia aliwahamasisha vijana kutumia kikamilifu fursa za mikopo zinazotolewa kupitia Halmashauri kwa ajili ya kukuza shughuli zao za kiuchumi. Alieleza kuwa mikopo hiyo inaweza kuwa chachu ya kujiajiri, kuongeza kipato na kuimarisha ustawi wa maisha yao endapo itatumika kwa malengo yaliyokusudiwa.
Kwa upande wa matumizi ya teknolojia, Simba aliwataka vijana kuepuka matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii ambayo yanaweza kusababisha migogoro au kuathiri maadili ya jamii. Badala yake, aliwahimiza kuitumia mitandao hiyo kama nyenzo ya kujifunza, kufanya biashara na kutafuta fursa mbalimbali za kujiongezea kipato.
Alisema katika dunia ya sasa ya kidijitali, mitandao ya kijamii inaweza kuwa nyenzo muhimu ya maendeleo ikiwa itatumika kwa malengo chanya na yenye tija kwa vijana na taifa kwa ujumla. Hivyo, aliwataka kuwa mabalozi wazuri wa maendeleo kwa kutumia teknolojia katika kujenga uchumi wao na wa jamii inayowazunguka.
Naye Mbunge wa Jimbo la Ulanga, Salim Hashim, aliwahimiza vijana kutumia fursa zinazopatikana kupitia Halmashauri na taasisi mbalimbali za maendeleo. Alisema ofisi yake imeandaa mpango wa mikopo isiyo na riba unaolenga kuwawezesha vijana kuanzisha na kuendeleza biashara zao, kuimarisha uzalishaji mali, kupunguza changamoto za ajira na kuongeza ushiriki wao katika maendeleo ya wilaya na taifa kwa ujumla.



0 Reviews