Serikali Yapiga Marufuku Mikutano ya Hadhara na Maandamano Nchini

Serikali Yapiga Marufuku Mikutano ya Hadhara na Maandamano Nchini

Size
Price:

Read more


Serikali imetangaza msimamo mkali dhidi ya mipango ya maandamano haramu yasiyo na kibali na kubainisha kuwa haitamfumbia macho wala kumuonea huruma mtu yeyote anayehusika katika kipindi hiki. 

Akitoa taarifa hiyo bungeni jijini Dodoma leo Juni 26, 2026, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Patrobas Katambi, amefichua kuwa tayari Jeshi la Polisi limekamata watu kadhaa na linatarajia kuanza kuwahoji ili kuchukua hatua stahiki. 

Hatua hii imekuja baada ya Mbunge wa Dodoma, Pascal Chinyele, kuomba mwongozo wa Spika kwa kutumia Kanuni ya Kudumu ya 79 akitaka ufafanuzi wa serikali kuhusu matishio ya maandamano yanayosambaa kwenye mitandao ya kijamii.

Katika kukabiliana na matishio hayo ya uvunjifu wa amani, serikali imepiga marufuku mikutano yote ya hadhara ya vyama vya siasa nchini. 

Waziri Katambi amemuagiza Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, Camillus Wambura, kusitisha utoaji wa vibali vya mikutano ya hadhara ili kuruhusu vyombo vya usalama kujielekeza kikamilifu katika kudhibiti vitisho hivyo vinavyoratibiwa na baadhi ya watu mtandaoni.

 Aidha, IGP Wambura ametakiwa kuwaelekeza Makamanda wa Polisi wa mikoa, wilaya, na polisi kata kuweka mikakati madhubuti ya ulinzi kwenye maeneo yao.

Sambamba na mikakati hiyo, Waziri Katambi ameagiza kufungwa kwa baadhi ya sehemu za starehe zenye viashiria vya uvunjifu wa amani, hususan katika maeneo ya Masaki na Oysterbay mkoani Dar es Salaam pamoja na maeneo mengine yanayohusika. Ili kuimarisha usalama zaidi, serikali imetoa agizo la lazima kwa kila mgeni anayelala katika nyumba za kulala wageni kote nchini kuandikishwa kwenye daftari maalumu kwa kutumia Kitambulisho cha Taifa cha NIDA.


222222@@@@@@@@@@@@@


WAKIMBIZI WAWAKUMBUSHA WATANZANIA KUTOCHEZEA AMANI


Wakimbizi wapatao 155,811 wanaohifadhiwa katika maeneo mbalimbali nchini wameiomba Serikali ya Tanzania chini ya Rais Samia Suluhu Hassan pamoja na wananchi wote kuendelea kulinda amani iliyopo, wakibainisha kuwa kukosekana kwa amani kunasababisha watu kupoteza kila kitu na kulazimika kukimbilia nchi nyingine na kwamba yaliyowakuta wao ni mfano hai.


Wakimbizi hao wametoa kauli hiyo jijini Dar es Salaam wakati wa maadhimisho ya Siku ya Wakimbizi Duniani, ambayo huadhimishwa kila mwaka mwezi Juni, yakiwa na kaulimbiu isemayo “Hadi Kila Mtu Awe Salama”.


 Walitoa shukrani za dhati kwa Rais Samia Suluhu Hassan, na wananchi kwa ujumla kwa kuendelea kuwapa hifadhi na usalama bila ubaguzi.


Akizungumza katika maadhimisho hayo, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Patrobas Katambi, amesema Tanzania inapaswa kujifunza kutokana na hali zilizotokea katika nchi jirani na kuendelea kuimarisha mazingira ya amani na utulivu.


Amesema serikali itaendelea kuwahudumia wakimbizi waliopo nchini na kuhakikisha usalama wao, huku akisisitiza kuwa amani ni msingi muhimu unaowezesha wananchi kujikita katika shughuli za uzalishaji na maendeleo ya kiuchumi.


Alieleza kuwa ni agizo la Rais Samia kuwa serikali itaendelea kuwahudumia wakimbizi wote waliopo nchini kwa kuzingatia utu na haki za binadamu.


Alikumbusha kuwa msimamo wa Tanzania kwa sasa ni kuhimiza urejeaji wa hiari wa wakimbizi kwenda maeneo salama kama suluhisho bora zaidi.



SERIKALI YAAGIZA WAFUGAJI WALIOSHINDA KESI WALIPWE FIDIA


Serikali imezielekeza Wizara ya Fedha kwa kushirikiana na Wizara ya Maliasili na Utalii kuhakikisha wanawarejeshea haraka wafugaji mifugo yao au kuwapa fidia stahiki wale wote walioshinda kesi mahakamani baada ya kutaifishiwa mali zao. 

Agizo hilo limetolewa leo bungeni jijini Dodoma wakati wa kuhitimisha mkutano wa tatu wa Bunge ambalo limeahirishwa hadi Agosti 25, mwaka huu.

Hatua hiyo inakuja baada ya kubainika kuwa baadhi ya wafugaji katika maeneo mbalimbali walitaifishiwa mifugo yao baada ya kukamatwa kwenye maeneo yaliyohifadhiwa, lakini baada ya kwenda mahakamani na kushinda mashauri hayo, taasisi husika zimeshindwa kutekeleza maamuzi ya kisheria. 

Badala yake, taasisi hizo zimekuwa zikitoa sababu zisizo na tija kama vile kudai kuwa mifugo hiyo ilikufa au kupotea, jambo linalodhoofisha sekta ya mifugo na kuwaacha wananchi katika ufukara mkubwa. 

Serikali imesisitiza kuwa kama mifugo hiyo ilikufa au kupotea, ni lazima wafugaji hao warejeshewe fidia kamili ya thamani ya mali zao ili kulinda misingi ya utawala wa kisheria na utoaji haki.

Ili kukomesha kabisa changamoto hiyo, Serikali imetangaza kuwa katika mkutano ujao wa Bunge, itawasilisha mapendekezo ya marekebisho ya sheria zinazosimamia utaifishaji wa mifugo na mali kwenye maeneo yaliyohifadhiwa kwa lengo la kuifuta kabisa sheria hiyo.

Mbali na suala la mifugo, viongozi na watendaji nchini wametakiwa kuchapa kazi kwa bidii na kuendelea kutekeleza majukumu yao ya kila siku badala ya kupunguza kasi kwa kusubiri teuzi mpya, maarufu kama "mkeka" au "PDF". 

Zipo taarifa zinazoonesha kuwa baadhi ya viongozi wamepigwa ganzi na kulegeza utendaji wakisubiri mabadiliko ya nafasi za uongozi, jambo linalosababisha huduma za umma kudorora. Serikali imeonya kuwa watendaji wote watakaobainika kusubiri teuzi badala ya kuwahudumia wananchi wataondolewa mara moja na nafasi zao kuchukuliwa na watu wenye utayari wa kufanya kazi, kwani shughuli za umma hazitakiwi kusimama kwa sababu ya watu wachache wanaosubiri "mkeka".

Katika hatua nyingine, viongozi wa mamlaka za serikali za mitaa wamekumbushwa kuwa utatuzi wa kero za wananchi ni jukumu lao la kila siku na hawapaswi kusubiri ziara za viongozi wa kitaifa ili kutatua changamoto za msingi. 

Ziara za viongozi wa ngazi za juu sio mbadala wa utendaji wa serikali za mitaa, hivyo wizara, idara, na sekretarieti za mikoa zimeelekezwa kuhakikisha mifumo ya kuanzia ngazi ya mtaa na kijiji inafanya kazi ipasavyo. 

Taasisi zote zimetakiwa kutenga muda maalum wa kusikiliza changamoto za utoaji huduma, na viongozi wote watapimwa kwa namna wanavyotekeleza maagizo yanayotolewa.

Aidha Serikali imebainisha mpango wa kuondoa uchaguzi wa kila mwaka wa nafasi za Naibu Meya na Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri, ambao umekuwa ukigharimu fedha nyingi, kuchochea migongano, na kuzorotesha utulivu wa kiutendaji. Katika mkutano ujao wa Bunge, yatawasilishwa mapendekezo ya kubadilisha mfumo huo ili viongozi wa nafasi hizo waweze kuongoza kwa kipindi chote cha uhai wa Baraza la Madiwani. 

Marekebisho haya ya sheria yanatarajiwa kuleta utulivu wa kisiasa na kiutendaji, na kuwawezesha viongozi kujielekeza kikamilifu katika shughuli za maendeleo ya wananchi katika maeneo yao.

0 Reviews

Contact form

Name

Email *

Message *