Katika kile kinachoonekana kama msimamo thabiti wa kulinda heshima na uwezo wa Mtanzania, Katibu Mkuu wa Chama cha Ukombozi wa Umma (CHAUMMA), Salim Mwalimu Juma, amekemea vikali tabia ya baadhi ya watu kudharau mawazo ya wataalamu na viongozi wa ndani na kusubiri kauli kutoka kwa wageni ili kukubali ukweli.
Salim amebainisha kuwa ni jambo la kusikitisha kuona ujumbe wa msingi uliotolewa na Jaji Mstaafu Mohamed Chande Othman unapuuzwa na baadhi ya watu, lakini watu hao hao wangekuwa wepesi kuukubali na kuushangilia kama ungetoka kinywani mwa "Mzungu".
Amesisitiza kuwa matatizo yanayoikabili nchi yetu, ikiwemo hitaji la mabadiliko ya katiba, tume huru ya uchaguzi, na changamoto za ajira, ni masuala yetu ya ndani ambayo yanahitaji utatuzi wa Kitanzania na si maelekezo kutoka nje ya mipaka yetu.
Mwalimu Juma ameshambulia fikra duni (mentality) ya kuhitaji uthibitisho wa mataifa ya Magharibi ili tuamini ukubwa wa matatizo yetu au uhalali wa madai yetu, akisema kuwa ni dharau kwa akili na utashi wa Watanzania.
Anasema kuwa kama kweli tunatambua kuwa changamoto hizi ni sugu, hatupaswi kusubiri mtu atoke nje ya nchi aje kutuambia kile ambacho tayari tunakijua tangu mchakato wa uchaguzi wa Oktoba 29 na madai ya katiba ya muda mrefu.
Katibu huyo mkuu ameweka wazi kuwa uwezo wa kutatua changamoto zetu tunao na umedhihirika mara nyingi kupitia ubunifu wa ndani.
Salim Mwalimu Juma anasema watu wa ndani wanaelewa changamoto kwa undani zaidi kuliko mgeni yeyote, hivyo suluhisho la kudumu lazima litoke ndani ya nyumba.
Anatoa wito kwa Watanzania kuwa wazalendo, kupenda vya nyumbani, na kukataa kutumiwa vibaya na wanaharakati au viongozi wanaojivika uzalendo wakati ndani ya nafsi zao wanategemea hisani na maelekezo ya watu wa nje ili kutoa maamuzi.
Ujumbe uko wazi kuwa maendeleo ya Tanzania na amani yake vitalindwa na Watanzania wenyewe kupitia maridhiano na majadiliano ya dhati, na si kupitia kelele za mtandaoni au shinikizo la wageni. Kwa kuimarisha mifumo yetu ya ndani na kuaminiana, tunaweza kupata katiba itakayotokana na matakwa ya wananchi wenyewe, jambo ambalo litathibitisha kuwa Tanzania ni nchi huru inayojitegemea kifikra na kimatendo.
