MNAOLAZIMISHA MAJINA NA USHAHIDI WA TUME UWEKWE WAZI MNA NINI?


Ni lazima kujiuliza, ni nini hasa kiko nyuma ya pazia kwa wale wanaopambana usiku na mchana kulazimisha ushahidi na majina ya mashahidi wa Tume ya Jaji Chande yawekwe hadharani? Je, ni kwa maslahi gani na kwa faida ya nani? Ni sheria gani za ndani au mikataba gani ya kimataifa inayoruhusu kuanika majina ya waathirika na mashahidi nyeti kabla hata ya hatua za kisheria kuanza? Hili ni swali ambalo kila Mtanzania mzalendo anapaswa kujiuliza, hasa unapoona watu hawa wanajaribu kuiponda ripoti kwa matusi na kashfa.

Tangu Ripoti ya Tume iliyoongozwa na Jaji Mstaafu Mohamed Chande Othman iwasilishwe Aprili 23, 2026, maoni mengi chanya yametolewa yakimpongeza Mheshimiwa Rais Samia Suluhu bHassan kwa busara ya kuiunda na kuipongeza Tume yenyewe kwa weledi wa hali ya juu. 

Ripoti hii imekuwa na nguvu kwa sababu imetumia njia za kisayansi (methodology) kufikia waathirika wa kweli—wale waliopoteza ndugu, walioumia, na waliopoteza mali Oktoba 29, 2025. Sasa, kwanini kuna kundi linataka kuvuruga utulivu huu kwa kulazimisha "uwazi" usio na tija?

Inawezekana kabisa kuwa wanaolazimisha mambo haya ni wale wanaofahamu fika kuwa hawatakwepa mkono wa sheria. Hawa ni wale ambao walipanga, walioratibu, waliofadhili, na waliochochea vurugu hizo, na sasa wanajua kuwa ripoti imewaumbua. Kwa kulazimisha ushahidi uwekwe wazi, wanatafuta fursa ya kwenda kuvuruga ushahidi huo na kuwadhuru mashahidi, kama ambavyo tumewahi kushuhudia katika mataifa mengine yaliyopitia mizozo ya namna hii.

Lengo lao ni baya na ni la hatari kwa mustakabali wa nchi yetu. Wanataka kuturudisha tulipotoka, ili nchi ionekane haitawaliki kama walivyokusudia tangu mwanzo. Walishatuletea vurugu zilizotuumiza, biashara zetu zikadorora, na sasa taifa linapambana kurekebisha hali hiyo huku kukiwa na changamoto za kiuchumi kutokana na migogoro ya Mashariki ya Kati. Watu hawa hawajali maumivu ya Watanzania, bali wanajali usalama wa ngozi zao.

Ripoti ya Tume ya Jaji Chande ni nyenzo muhimu ya uwajibikaji ambayo imetoa mapendekezo ya kuturejesha kwenye amani, umoja, na mshikamano. Tuwaambie kwa nguvu zote watu hawa: Watuache! Tuna shida nyingi ambazo wao wenyewe walitusababishia, na sasa tunataka kuzitatua kwa amani na kwa mujibu wa sheria za nchi yetu. Hakuna ushahidi wa jinai unaowekwa sokoni, na mashahidi wetu watabaki kulindwa ili haki itendeke bila woga wala upendeleo.

BOSS TV

Hii ni Official blog ya BOSS MEDIA kwa habari za siasa, jamii, elimu, burudani na michezo tufuatilie kwa uhakika zaidi

Post a Comment

Previous Post Next Post