Na Mwandishi Wetu
DODOMA: Katika maisha ya kawaida, watu wengi huchukulia amani kama jambo la kawaida lisilohitaji kufikiriwa sana. Hata hivyo, kwa wale waliowahi kukumbana na madhira ya vurugu na machafuko, amani huwa na thamani kubwa isiyoweza kupimika.
Mkazi wa Mbabala mkoani Dodoma, Paschazia, ni miongoni mwa watu walioguswa moja kwa moja na athari za kukosekana kwa amani. Anasema wazi kuwa mtu ambaye hajawahi kupitia madhira ya vurugu hawezi kuelewa kwa undani umuhimu wa amani iliyopo nchini.
Akisimulia uzoefu wake, Paschazia anaeleza kuwa watu wengi, hasa vijana, hujiingiza katika vurugu wakiamini kuwa hawana cha kupoteza. Hata hivyo, anasisitiza kuwa mtazamo huo si sahihi, kwani matokeo ya kukosekana kwa amani huathiri kila mtu bila kujali hali yake.
Kwa mujibu wake, pale amani inapopotea, hakuna anayekuwa salama, na wala hakuna sehemu ya kukimbilia kwani kila mtu hutegemea nchi yake kama makazi ya mwisho.
“Watu wengi wanaingia katika vurugu wakisema hawana cha kupoteza, lakini hawajui kwamba amani ikitoweka hakuna mtu atakayekimbia nchi yake. Hatu¬na nchi nyingine ya kukimbilia,” anasema Paschazia.
Anasisitiza kuwa amani ndiyo msingi wa kila kitu katika maisha ya binadamu na maendeleo ya taifa. Bila amani, shughuli za kiuchumi husimama, huduma za kijamii huvurugika na maisha ya watu hubadilika kwa ghafla.
Paschazia anatoa ushuhuda wake binafsi kueleza ukubwa wa madhara ya vurugu. Anasema wakati wa matukio ya vurugu yaliyotokea Oktoba 29, nyumba yake ilichomwa moto na kusababisha hasara kubwa ya mali.
Katika tukio hilo, alipoteza gari aina ya Hiace lililokuwa na thamani ya zaidi ya shilingi milioni 50. Aidha, nyumba yake iliteketea kwa moto na kusababisha hasara inayokadiriwa kufikia zaidi ya shilingi milioni 150.
Mbali na hayo, alieleza kuwa alipoteza mali nyingine muhimu ikiwemo seti tatu za sofa, friji mbili pamoja na vitu vingine vya thamani vinavyokadiriwa kuwa zaidi ya shilingi milioni 25.
“Nimepoteza vitu vingi sana vya thamani. Ni tukio ambalo siwezi kulisahau kirahisi, na limenifundisha umuhimu wa amani kwa njia ngumu,” anasimulia kwa masikitiko.
Hata hivyo, Paschazia anashukuru juhudi za pamoja zilizofanywa na askari Polisi, viongozi wa mtaa pamoja na majirani walioweza kusaidia kudhibiti moto huo kabla haujasambaa zaidi na kuharibu kila kitu.
Anasema msaada huo ulipunguza kwa kiasi fulani ukubwa wa hasara ambayo ingeweza kuwa mbaya zaidi kuliko ilivyotokea.
Kupitia uzoefu wake, Paschazia anatoa wito kwa vijana na jamii kwa ujumla kulinda amani na kuepuka kushiriki katika vitendo vya vurugu. Anaamini kuwa ni jukumu la kila mwananchi kuhakikisha nchi inaendelea kuwa salama na yenye utulivu.
Kwa ujumla, simulizi yake ni funzo kwa wengi kuwa amani si jambo la kawaida bali ni rasilimali muhimu inayopaswa kulindwa kwa gharama yoyote. Ni pale tu mtu anapopitia madhira ndipo anaweza kuelewa kwa kina thamani ya amani katika maisha yake.
