“Yanayodaiwa kuwa maandamano hayakuzingatia matakwa ya Ibara ya 18 na 20 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (1977) na sheria za nchi ikiwemo maandamano kuwa ya amani na kutoa notisi kwa Jeshi la Polisi kwa mujibu wa vifungu vya 42 na 43 vya Sheria ya Jeshi la Polisi na Huduma Saidizi.”
“Haki ya kila mtu kushiriki uchaguzi kama mpiga kura au mgombea ni haki ya kikatiba kwa mujibu wa Ibara ya 5 ambayo haipaswi kupokwa.”
“Ghasia zilipangwa na kutekelezwa siku iliyotangazwa kisheria kuwa ni siku ya Uchaguzi Mkuu. Hivyo, kufanya ghasia siku hiyo ilikuwa ni kupoka haki ya Kikatiba na Kisheria za wananchi wengine ikiwemo haki ya kupiga na kupigiwa kura”
“Washiriki wa ghasia za wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu walibeba silaha za aina mbalimbali zikiwemo mawe, nondo, mkuki, sururu, fimbo, marungu, visu, viberiti, vilipuzi, bunduki, manati, kombeo, rato na mapanga jambo ambalo haliruhusiwi kisheria katika maandamano ya amani.”
“Hii ni kinyume na sheria na taratibu za Kimataifa (Ibara ya 21 ya Mkataba wa Haki za Kiraia na Kisiasa, 1966), Kikanda (Ibara ya 11 ya Mkataba wa Afrika wa Haki za Watu na Binadamu, 1981 na Ibara ya 10 na 11 ya Mkataba wa Ulaya wa Haki za Binadamu, 1950) na Kitaifa (Ibara ya 18 na 20 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, 1977) haziruhusu maandamano ya watu waliobeba silaha; na;”
“Sheria na taratibu za Kimataifa, Kikanda na Kitaifa haziruhusu maandamano yanayosababisha taharuki katika jamii, kuhatarisha usalama wa Taifa, kusababisha uharibifu wa mali za umma na binafsi pamoja na kuhatarisha maisha ya watu wengine. Mambo hayo yakifanyika, yanakuwa kinyume cha tafsiri ya maandamano ya amani.”
“Kwa kuzingatia sheria na kanuni zinazotawala maandamano ya amani kimataifa, kikanda na kitaifa na ushahidi uliowasilishwa mbele ya Tume, ni maoni ya Tume kuwa kilichotokea wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu wa tarehe 29 Oktoba, 2025 hakikuwa maandamano ya amani na hivyo kuwa nje ya kinga za sheria na kanuni hizo.”
