BILA AMANI HATA WATU WA HALI YA CHINI TUSINGEFIKIWA


KIONGOZI wa waendesha bodaboda Ilala, Zulkif Kimaro, amesisitiza umuhimu wa amani nchini akieleza kuwa bila kuwepo kwa utulivu, hata wananchi wa hali ya chini wasingeweza kunufaika na huduma mbalimbali zinazotolewa na serikali. Kauli hiyo ameitoa akirejea matukio yaliyotokea Oktoba 29, 2025, akiyataja kuwa ni funzo muhimu kwa mustakabali wa taifa.

Kimaro amesema kuwa amani imekuwa nguzo kuu inayowezesha wananchi wa kada zote kufikiwa na fursa za maendeleo, ikiwemo kutengewa maeneo rasmi ya kufanyia biashara kama bodaboda. Kwa mujibu wake, mazingira ya utulivu yamechangia kwa kiasi kikubwa kuwainua watu wengi kiuchumi, hasa wale waliokuwa katika hali ya chini.

“Amani ndiyo kila kitu. Kama tume inavyohimiza wananchi kutoa maoni yao kuhusu yaliyotokea Oktoba 29, ni muhimu kila mmoja kushiriki ili ukweli ujulikane. Sote tunahitaji kuona nchi yetu inaendelea kuwa na amani, kwani bila hiyo hatuwezi kusonga mbele,” amesema Kimaro.

Akizungumzia uzoefu wake binafsi, Kimaro amesema kuwa kama mzaliwa wa Buguruni, ameweza kufikiwa na kutoa maoni yake kwa tume husika kuhusu namna bora ya kuhakikisha amani ya kudumu inapatikana. Amehoji kuwa pasipo amani, isingekuwa rahisi kwa viongozi kuwafikia wananchi wa kawaida na kusikiliza maoni yao.

“Ni muhimu kuendelea kuitunza amani yetu kwa sababu ndiyo inayotuwezesha kuishi kwa utulivu, kufanya kazi zetu na kulea familia zetu kwa upendo. Bila amani, maisha yangekuwa magumu sana kwa kila mmoja wetu,” ameongeza.

Hata hivyo, Kimaro amegusia pia suala la baadhi ya vijana kushiriki katika maandamano yasiyo na tija, akieleza kuwa huenda baadhi yao walikuwa wanakabiliwa na changamoto za afya ya akili. Ameiomba serikali kuzingatia umuhimu wa afya ya akili kwa vijana ili kuwasaidia kufanya maamuzi sahihi.

“Siyo jambo baya kwa serikali kuweka utaratibu wa kupima afya ya akili kwa vijana mara kwa mara. Hii itasaidia kubaini changamoto zilizopo na kuchukua hatua mapema kabla hazijaleta madhara makubwa kwa jamii,” amesema.

Kwa kuhitimisha, Kimaro ametoa wito kwa Watanzania wote kuendelea kulinda na kuthamini amani iliyopo nchini, akisisitiza kuwa ndiyo msingi wa maendeleo, mshikamano na ustawi wa jamii nzima.

BOSS TV

Hii ni Official blog ya BOSS MEDIA kwa habari za siasa, jamii, elimu, burudani na michezo tufuatilie kwa uhakika zaidi

Post a Comment

Previous Post Next Post