Na Mwandishi Wetu
MSANII wa filamu za Bongo Movie, Daniel Lufingo, amesema kuwa amani katika jamii ni nguzo muhimu kwa ukuaji na ustawi wa sekta ya sanaa, akisisitiza kuwa wasanii hawawezi kufanya kazi kwa ufanisi bila kuwepo kwa mazingira tulivu na yenye mshikamano.
Lufingo, anayefahamika zaidi kama Adam kutoka tamthilia maarufu ya Noma, alieleza kuwa amani ya kweli haiwezi kupatikana bila haki, akibainisha kuwa misingi hiyo miwili inategemeana katika kujenga jamii imara.
“Amani ni tunda la haki. Mtu mmoja anapotimiza wajibu wake kwa mwingine, ndipo amani hupatikana. Huwezi kutenganisha amani na wajibu katika ustawi wa jamii yoyote,” amesema.
Akiangazia mchango wa sanaa katika jamii, Lufingo amesema kuwa wasanii wanategemea sana ushirikiano wa wananchi pamoja na serikali ili kuweza kuendeleza kazi zao. Ameonya kuwa kukosekana kwa amani kunaweza kusababisha kusimama kwa shughuli za kisanii na kuathiri maendeleo ya sekta hiyo.
“Sisi wasanii tunahitaji jamii kwa sababu ndio wateja wetu, lakini pia tunahitaji mahusiano mazuri na serikali ambayo ni mlezi wetu. Kukosekana kwa amani kunasababisha kazi zetu kusimama na wakati mwingine tunajikuta kwenye njia panda,” ameongeza.
Akizungumzia hali ya sasa ya taifa, msanii huyo alibainisha kuwa nchi inaendelea kujijenga upya kufuatia changamoto zilizojitokeza baada ya uchaguzi uliopita wa Oktoba 29. Alisisitiza umuhimu wa kila mwananchi kushiriki katika kurejesha mshikamano wa kitaifa kwa kutimiza wajibu wake ipasavyo.
“Kwa sasa nchi inapambana kuponya majeraha ya uchaguzi uliopita, hivyo kila mmoja ana jukumu la kuchangia ujenzi wa upya wa umoja wa kitaifa,” amesema.
Kuhusu nafasi ya vijana, Lufingo amewahimiza kushiriki kikamilifu katika masuala ya kisiasa na maendeleo ya nchi, akieleza kuwa wao ndio nguvu kazi ya sasa na ya baadaye.
“Vijana tuache kusema siasa ni uongo. Siasa ndiyo inaongoza maisha yetu, hivyo tushiriki kikamilifu na tuepuke ubaguzi wa kidini, kikabila au kisiasa ambao ni sumu kwa umoja wetu,” amesisitiza.
Aidha, alieleza kuwa tofauti za kijamii hazipaswi kuwa kikwazo cha maendeleo, hasa katika zama hizi za elimu na uelewa mpana. Aliongeza kuwa wasanii wana jukumu la kipekee katika jamii, si tu kuburudisha bali pia kuelimisha na kuunganisha watu.
“Wasanii ni kioo cha jamii na daraja linalounganisha watu. Tunawajibika kuelimisha, kuburudisha na kushauri,” amesema.
Hata hivyo, Lufingo amekiri kuwa baadhi ya wasanii bado wanakabiliwa na changamoto mbalimbali zinazowafanya kusita kutoa maoni yao hadharani, ikiwemo masuala ya usalama na udhibiti wa maudhui.
Akigusia haki za vijana, alisisitiza umuhimu wa kuwapa nafasi ya kusikilizwa na kushirikishwa katika maamuzi ya kitaifa, huku akihimiza matumizi ya njia za mazungumzo jumuishi katika kudai haki.
Kwa upande wake, ameishauri serikali kuendelea kushirikisha wananchi katika maamuzi muhimu ya kitaifa na kutambua mchango wa wasanii wakati wote, si wakati wa kampeni pekee.
“Serikali itambue kuwa wasanii ni sehemu muhimu ya maendeleo ya taifa, si wakati wa kampeni tu bali wakati wote,” amesisitiza.
Akihitimisha, Lufingo ametoa wito kwa vijana na Watanzania kwa ujumla kudumisha amani kwa kutimiza wajibu wao kwa nchi, akieleza kuwa ushirikiano kati ya raia na serikali ndio msingi wa amani ya kudumu.
“Kila mmoja atimize wajibu wake kwa nchi, na nchi itimize wajibu wake kwa raia. Hapo ndipo tutakapopata amani ya kweli,” amehitimisha.
